Kuhusu Sisi

Participatory Plantation Forestry Programme (PFP2)

Programu ya Panda Miti Kibiashara - (Participatory Plantation Forestry Programme PFP2) ni Programu inayohusisha Serikali za Tanzania na Finland. Programu inalenga katika kuinua kipato cha wananchi vijijini katika maeneo ya Nyanda za Juu Kusini mwa Tanzania kwa kuboresha upandaji miti ulio endelevu na kuongeza thamani ya mazao ya misitu. 

Moja ya malengo makuu ni kufadhili upandaji miti binasi kwa kuwapa kipaumbele wakulima wadogo ambao watasaidiwa katika harakati za kuanzisha Vikundi vya Wakulima wa Miti (Tree Growers’ Associations - TGAs) ili waweze kunufaika wanapoingia kwenye masoko ya mbao. 

Katika kuhakikisha usimamizi bora wa kilimo cha miti katika siku zijazo, Programu imeandaa mpango madhubuti wa kujenga uwezo katika ngazi zote za misitu kuanzia upandaji wa miti mpaka kwenye masoko ya mazao ya misitu. Pia mpango huu wa uwezeshaji utalenga masuala ya ajira katika sekta ya misitu katika Nyanda za Juu Kusini. 

Ili kuinua maendeleo ya kijamii katika Nyanda za Juu Kusini, Programu itazingatia ushirikishi wenye kuzingatia usawa wa kijinsia na kuimarisha haki za makundi maalum kwa kuhakikisha kuwa yanapewa nafasi ya kushiriki katika mchakato mzima wa mpango wa matumizi ya bora ya ardhi.

 Katika kuhakikisha uhifadhi endelevu wa mazingira, Programu imejumuisha uhifadhi wa viumbe hai katika Mpango wa Matumizi Bora ya Ardhi na kuboresha usimamizi wa viumbe hai katika maeneo ya upandaji miti.

Mbinu mpya za Progamu zitafanyiwa thathimini na zile zitakazothibitika kuwa bora zaidi zitatumika katika sekta nzima ya misitu ili kuhakikisha matumizi endelevu ya rasilimali  za misitu na kuongeza faida kutokana na rasilimali hizo.  Programu itawezesha maendeleo makubwa katika sekta hii kwa kuanzisha na kushiriki katika majadiliano baina ya wadau wakubwa wa sekta hii na kutoa mapendekezo juu ya utayarishaji wa sera, sheria na maendeleo ya biashara.

Progamu  inafanya kazi chini ya uangalizi wa Wizara ya Maliasili na Utalii ya Tanzania na Ubalozi wa Finland uliopo Dar es Salaam. Programu imepangwa kuwa ya miaka 16, na kwa sasa ipo katika awamu ya kwanza (2014-2017). Awamu hii ambayo inatekelezwa na shirika la Indufor Oy la Finland kwa ushirikiano na Niras, ambayo yanatoa msaada wa huduma za kitaalam za upandaji miti kibiashara kwa ujumla.

Dira

Dira ya Programu kwa sekta ya upandaji miti kibiashara Tanzania, ni kuwezesha uzalishaji wa kipato endelevu kwa jamii nzima katika sekta ya misitu na sekta nyingine amabatanishi huku ustawi endelevu wa jamii na mazingira ukizingatiwa katika uwekezaji huo.

Hii itaifanyaTanzania kuwa mzalishaji mkuu wa mbao kwa masoko la ndani na nje, na wawekezaji katika sekta ya upandaji miti na viwanda vya misitu wataziona Nyanda za Juu Kusini  kuwa ni moja ya maeneo muhimu na yenye tija  kwa  uwekezaji .

Dhamira

Lengo kuu la Programu ni upandaji miti endelevu kwa shabaha ya kuondoa umaskini na kukuza uchumi nchini.

Dhamira kuu ya Programu hii, ni kuanzisha na kuimarisha upandaji miti kibiashara ulio endelevu na jumuishi ili kuchangia katika kuinua kipato cha watanzania na kupunguza umasikini.

Katika harakati za kuwezesha wakulima wa miti wa Nyanda za Juu Kusini kuongeza kipato na ajira, haki za makundi maaluum zitalindwa na kuwawezesha kushiriki tangu hatua za awali za upandaji  miti hadi uuzaji wa mazao sokoni.

Lengo la awamu ya kwanza ya Programu hii (2014-2017), ni kuwezesha upandaji wa miti ulio endelevu, shirikishi na wenye faida kiuchumi na kuhakikisha kwamba shughuli ambatanishi zinatoa ajira  na kuongeza kipato kwa wamililiki  binafsi wa mashamba  ya miti, vikundi vya uzalishaji vidogo na vya kati na kaya za wasiojiweza zilizo katika eneo la Programu.